Wednesday , 30th Jan , 2019

Shule ya Sekondari ya Anna Mkapa iliyopo Kata ya Pasua katika Manispaa ya Moshi imebainika kufanya udanganyifu kwa kushiriki kuhujumu miundombinu ya maji kwa mamlaka ya Majisafi na Mazingira mjini Moshi (MUWSA) kinyume cha sheria.

Tukio hilo lilibainika jana usiku majira ya saa 3:30 baada ya wafanyakazi wa MUWSA kufanya operesheni ya kushtukiza katika shule hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema waliotoa taarifa kwa mamlaka juu ya wizi huo.

Akizungumza katika eneo la tukio, Afisa Habari wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA), Rashid Nachan alisema kilichofanyika ni wizi na kwamba wahusika wanachangia kuhujumu uchumi wa nchi.

“Kinachoonekana hapa dhahiri ni kwamba uongozi wa shule unafahamu kinachoendelea, kwa sababu hawezi kuja mtu kutoka nje kufanya kitendo cha kuondoa mita na kuweka bomba la moja kwa moja bila uongozi wa shule kufahamu atakuwa anafanya kwa faida ya nani sasa", alihoji Nachan.

Akijibu tuhumza hizo Mkuu wa Shule hiyo, Sindato Seiya amesema, “nimeiona sehemu yenyewe na toka jana usiku huyu fundi ametafutwa na hapokei simu hadi sasa maana yake anajua mwenyewe ni kitu gani amefanya hapa shuleni".