Thursday , 17th Mar , 2016

Kiwanda cha Saruji cha Tembo kilichopo jijini Mbeya kimetoa msaada wa mifuko 1,000 ya saruji na mashine nne za kufyatuliwa matofali kwa shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga ambayo Mabweni ya Shule hiyo yaliungua moto.

Muonekano wa bweni la Wavulana katika shule ya sekondari Iyunga jijini Mbeya mara baada ya kuteketea kwa moto

Akikabidhi msaada huo kwa uongozi wa halmashauri ya jiji la Mbeya,Meneja Uajiri watu wa kiwanda cha saruji cha Tembo,Grayson Tarimo aliitaja shule ya Iyunga kuwa miongoni mwa shule nchini zilizo na mchango mkubwa katika kuzalisha wataalamu mbalimbali.

Tarimo amekitaja kiwanda chao kuwa miongoni mwa taasisi zinazoendelea kunufaika kwa kuajiri wataalamu waliosoma katika shule hiyo kabla ya kujiendeleza kimasomo mahali pengine.

Akipokea msaada huo kaimu mkurugenzi wa jiji la Mbeya Dk Samweli Lazaro amesema bado misaada zaidi inahitajika kwa wadau ili kuwezesha ukarabati wa mabweni yaliyoungua sambamba na kununua samani vikiwemo vitanda na magodoro.

Dk.Lazaro amesema takribani shilingi milioni 700 zinahitajika ili kukamilisha shughuli hiyo na hadi sasa halmashauri pekee imekwishachangia kiasi cha shilingi milioni 70.