Wednesday , 3rd Jul , 2019

Kesi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Jamii Forum Maxence Melo, na mwenzake Mike William, imeshindwa kuendelea leo Julai 3 Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya shahidi wa upande wa mashtaka kutofika mahakamani.

Maxence Melo (kushoto).

Wakili wa serikali Daisy Makakala amedai kuwa, kesi hiyo ya jinai namba 458 ya mwaka 2016, ilikuwa iendelee kwa kusikiliza ushahidi lakini shahidi aliyepaswa kutoa ushahidi hakuwepo mahakamani, hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi huo.

Kutokana na maelezo hayo hakimu mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Huruma Shahidi, ameiahirisha kesi hiyo hadi Agost 1, 2019, na kuutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi mahakamani hapo ili kesi hiyo iweze kuisha.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Desemba 9 mwaka 2011 na Desemba 13 mwaka 2016, katika eneo la Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni, ambapo washtakiwa wanadaiwa kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini, na kosa la kushindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kuzuia taarifa binafsi za wateja wa mtandao wao.