Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde leo (Jumanne) Bungeni wakati alipokuwa anajibu swali lililoulizwa na Mhe. Salim Mwinyi Rehani Mbunge wa Uzini aliyetaka kufahamu kwamba ni lini serikali itaweza kuwatambua rasmi madereva wa bodaboda na bajaji kwa kuwaandikia mikataba, kulipiwa mifuko ya hifadhi ya jamii na waajiri wao.
"Serikali ilikwisha watambua rasmi madereva pikipiki, bodaboda au bajaji tangu mwezi Aprili mwaka 2009, ambapo pikipiki na bajaji zilikubaliwa kufanya biashara ya kusafirisha abiria kwa mujibu wa sheria. Ili madereva wa pikipiki au bajaji waweze kutambulika kiurahisi kwa lengo la kupatiwa huduma mbalimbali zikiwemo za hifadhi ya jamii kutoka serikalini na wadau wengine, serikali imefanya jitihada kubwa ya kuwahamasisha waunde vyama vyao", alisema Mavunde.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri aliendelea kwa kusema "nichukue fursa hii kutoa maagizo kwa watoa ajira wote nchini kwa vijana wanaoendesha Pikipiki au bajaji kuzingatia sheria ikiwa pamoja na kutoa mikataba ya kuhakikisha wanapata huduma nyingine muhimu ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kiufanisi na kuzingatia usalama wa uhai wao pamoja na vyombo vyao".
Kwa upande mwingine, Bunge la Tanzania lililoanza leo (Jumanne) limefanikiwa kuwaapisha wabunge wapya watatu ambao wote wanatoka CCM ni Damas Ndumbaro (Songea Mjini), Justin Monko (Singida Kaskazini) na Steven Kiruswa (Longido).


