Friday , 13th Nov , 2015

Mwanamama Petronila Simon mkazi wa Arusha mwenye mtoto mlemavu wa viungo na akili amelalamikia tabia ya kinababa kuwatelekeza kinamama pindi wanapojifungua watoto walemavu na kuwaacha bila kuwahudumia.

Mwanamama Petronila Simon mkazi wa Arusha mwenye mtoto Mlemavu wa viungo na akili alitelekezwa na Mzazi mwenzie

Mama huyo akizungumza kwa uchungu amesema kuwa alitelekezwa na mume wake anayejulikana kwa jina la Straton kuanzia mwaka 2008 huku akimtunza mtoto huyo katika hali ngumu ikiwemo kukosekana kwa chakula,matibabu na sehemu ya malazi hivyo amewaomba Watanzania wajitokeze kumsaidia mama huyo.

Kwa upande wao majirani akiwemo Saumu Athumani wameeleza kuwa mama huyo amekuwa akiishi maisha ya shida hata chakula na mahitaji mengine amekuwa akisaidiwa na majirani kutokana na ulemavu wa mtoto wake unaomlazimu kuwa karibu na kumuhudumia hivyo inakuwa vigumu kufanya shughuli za kujiingizia kipato hivyo wameiomba jamii imsaidie mama huyo.

Shabani Rashid ni Jirani anayeishi karibu na mama huyo ameiomba serikali iwasaidie kinamama wenye watoto walemavu ambao mara nyingi hukimbiwa na waume zao na kutelekezwa bila msaada wowote.

Matukio ya kinamama wanaojifungua watoto walemavu kutelekezwa na waume zao pamoja na kutengwa yamekithiri katika maeneo mengi nchini jambo ambalo linachochea ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto walemavu na kuzidisha unyanyapaa dhidi ya jamii ya walemavu, serikali pamoja na mashirika binafsi yana jukumu kubwa kutokomeza ukatili huu kwa watoto.

Mama huyo alifungua kesi katika mahakama ya mwanzo iliyoko jijini Arusha shauri namba 82 ambapo hukumu ilitolewa Oktoba 12 na mdaiwa kutakiwa kulipa shilingi 50,000 kila mwezi pesa ambazo hazitoshi kumhudumia mtoto huyo pamoja na matibabu ukizingatia gharama za maisha na uhalisia.