Thursday , 12th Nov , 2015

Wadau wa sekta ya madini nchini wameishauri serikali ya awamu ya tano kuboresha sekta ya madini ili kuweza kuleta ushindani kimataifa na kusaidia kukuza maendeleo ya haraka kwa wananchi.

Mshauri mwelekezi wa sekta ya madini kutoka kampuni ya MTL Consulting John-Bosco Tindyebwa.

Mshauri mwelekezi wa sekta ya madini kutoka kampuni ya MTL Consulting John-Bosco Tindyebwa amesema Tanzania imebarikiwa aina nyingi za madini hivyo ni kazi ya serikali kusimamia vizuri sekta hiyo ili kuwezesha wananchi pamoja na nchi kwa ujumla kupata maendeleo kwa kuwa rasilimali hiyo yaweza kukuza uchumi wa nchi kwa haraka kuliko sekta nyingine.

Aidha wadau wa habari kutoka maeneo yenye madini na yanayotarajiwa kujengwa migodi ya madini, wameshauri wananchi kupewa uelewa wa kutosha kuhusiana na uwekezaji hususani wa sekta ya madini kutokana na wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha na kuchangia migogoro au sintofahamu katika maeneo yanapoibuliwa madini.

Kwa upande wa wadau wa habari mkoani Morogoro wakiwemo waandishi wa habari, wameweza kuelimishwa kuhusiana na sekta ya madini, ikiwemo sheria ya madini ya mwaka 2010, vigezo na masharti ya utoaji wa leseni na vibali vya uchimbaji, usafishaji na uuzaji wa madini pamoja na namna ya serikali inavyoweza kunufaika na mirahaba hasa kwa kutoa asilimia ya pato ghafi inayotokana na uuzaji wa madini.