Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua kongamano la siku moja la wafanyabiashara baina ya Tanzania na India lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Amesema kwa sasa mwekezaji atafanya taratibu zote za uwekezaji katika kituo cha taifa cha uwekezaji cha TIC tofauti na hapo awali ambapo mwekezaji alilazimika kutembelea taasisi zaidi ya nne kwa ajili ya kukamilisha taratibu za uwekezaji.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Tanzania inawakaribisha wawekezaji ambao wapo tayari kuwekeza kwenye sekta ya Utalii, Madini, Miundombinu ya Mawasiliano na Uzalishaji wa Viwanda vidogo ambayo fursa zake zikowazi kwa ajili ya uwekezaji.
Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage amesema, Tanzania imechagua kushirikiana na India kwa kuwa nchi hiyo imefanikiwa kutokana na uwepo wa viwanda vidogo kwani asilimia 38 ya pato la India linatokana na viwanda vidogo, huku asilimia 45 ya bidhaa za India zinazouzwa nje ya nchini huzalishwa na viwanda hivyo.



