Mratibu wa Huduma za Maji, Afya na Mazingira kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi Bi. Theresia Kuiwete.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa itasaidia kupunguza idadi ya siku ambazo wanafunzi wa kike hulazimika kubaki nyumbani na hatimaye kuongeza mahudhurio na ufaulu wa wanafunzi wa kike katika shule mbali mbali nchini.
Mratibu wa Huduma za Maji, Afya na Mazingira kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi Bi. Theresia Kuiwete, amesema hayo leo na kwamba hatua hiyo itasaidia kupunguza bei na hivyo kuwezesha utekelezaji wa mpango wa ugawaji wa vifaa hivyo bure kwa wanafunzi nchi nzima kutokana na hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo wazazi.
"Kwa kweli hali ya upatikanaji wa huduma za hedhi salama kwa wanafunzi wa kike nchini sio nzuri, ukosefu wake umechangia idadi kubwa ya wanafunzi hao kutohudhuria masomo kwa wastani wa zaidi ya miezi miwili kila mwaka na hii imekuwa na athari kwa kiwango cha cha ufaulu na hata wengine kulazimika kuacha shule," amesema Bi. Kuiwete.
Kwa mujibu wa Bi. Kuiwete, ni kwa sababu hiyo ndiyo maana wadau wa elimu ya mtoto wa kike nchini wakaona ni bora kuja na kampeni itakayohamasisha uelewa na uchangiaji wa vifaa vya hedhi ili wanafunzi wa kike wapate fursa ya kuhudhuria mafunzo sawasawa na wenzao wa kiume.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Bi. Orsolina Tolage, amesema serikali inalipa kipaumbele suala la huduma ya hedhi salama kwa wanafunzi wa kike ambao wengi ufaulu wao umeshuka na hata kuacha masomo kutokana na hali hiyo.