Wednesday , 11th Jun , 2014

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo imekiri kuchelewa kutoa taarifa kuhusiana na kuruka kwa ndege maalum za utafiti ambazo huruka mpakani mwa Tanzania na Malawi na kuingia eneo la Tanzania na kusababisha hofu kwa wananchi wa maeneo hayo

Waziri wa uchukuzi nchini Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe.

Akitoa kauli ya serikali leo bungeni Mjini Dodoma Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa ndege hizo zimepewa vibali na vyombo vya udhibiti wa anga kuruka maeneo hayo na ndege hizo zinafuatiliwa kwa ukaribu,na kuongeza kuwa hazina madhara yoyote kwa wananchi kwani ni za kiutafiti na si vinginevyo.

Wakati huohuo, kampuni ya Reli Tanzania (TRL), leo imewamerudishiwa nauli zao zaidi ya abiria 1,200 waliokuwa wanaelekea Mikoa ya Kati na mingineyo kwa usafiri wa treni kutokana na kutetereka kwa daraja la reli kati ya stesheni ya Ruvu na mchepuko wa reli ya Ruvu kwenda Mruazi katika mkoa wa Pwani.

Wakizungumza na EastAfrica Radio kuhusiana na hatua hiyo abiria James na Mariam wamesema uongozi wa TRL umechelewa kutoa taarifa kwa wasafiri kuhusiana na kuahirishwa kwa safari hizo na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwao.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa TRL Midladjy Maez amesema
wataalamu wamepelekwa katika eneo hilo ili kufanya matengenezo baada ya kukamilika kwa matengenezo watatangaza tena kuanza kwa safari za reli ya kati.