Sunday , 10th Jan , 2016

Serikali imeuagiza uongozi wa wilaya halmashauri ya wilaya ya Kilosa kushughulikia haraka upimaji wa viwanja katika eneo la shamba la masugu, kata ya magomeni wilayani humo, ambalo limetengwa maalum kwa ajili ya waathirika wa mafuriko.

Mkurugenzi wa maafa ofisi ya waziri mkuu,Mbazi Msuya

Akizungumza mara baada ya kuwatembelea waathirika hao wa mafuriko wilayani Kilosa, mkurugenzi wa maafa ofisi ya waziri mkuu, Mbazi Msuya amesema kata ya Magomeni ipo bondeni na ardhi yake ni ya mchanga hali inayosababisha nyumba nyingi kuanguka pindi mafuriko yakijitokeza, kutokana na mto Mkondoa kujaa na kutema maji yake,

Msuya amegiza uongozi wa wilaya hiyo kupima haraka viwanja katika shamba hilo ili wakazi wa kata hiyo wahame kutoka katika bonde la mto kuepusha maafa zaidi yanayoweza kujitokeza.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa Iddi Mshiri, amesema zoezi la uhakiki wa wamiliki wa nyumba katika kata hiyo limeshaanza na kuwataka wakazi wote wenye hati miliki za nyumba zao wazifikishe wilayani ili wapatiwe viwanja.

Nao baadhi ya waathirika wa mafuriko hayo wakidai kuchelewa kupatiwa viwanja kwa awamu ya kwanza ndio kumechangia baadhi ya waathirika kushindwa kuhama mapema kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na kuiomba serikali kushughulikia mapema swala hilo ili maafa hayo yasijirudie tena