Friday , 27th Jun , 2014

Serikali ya Tanzania imesema kupitia mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inaendelea na ujenzi wa nyumba za walimu katika halmashauri 120 katika kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa walimu.

Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu TAMISEMI, Mhe. Kassim Majaliwa.

Hayo yameelezwa bungeni mjini Dodoma leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Mh. Kassim Majaliwa wakati akijibu swali katika kipindi cha mawali na majibu.

Katika maelezo yake, waziri Majaliwa amesema serikali imetenga shilingi bilioni 20 katika mwaka huu wa fedha katika kukamilisha mpango huo kwa kujenga nyumba katika halmashauri 40.

Awali, Mhe. Majaliwa wakati akijibu swali hilo amesema serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubaini mapungufu katika mpango wa awali wa mwaka wa fedha 2011-2012 wa kumlipa shilingi laki tano pamoja na samani za ndani kila mwalimu anayekwenda kufundisha katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na ubaguzi kwa watumishi wengine wanaofanya kazi katika sekta ya elimu.