Monday , 14th Mar , 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza kukusanya fedha kwa ajili ya kununua Meli mpya kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo Ziwa Victoria.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu alimnukuu rais kwa kusema “Rais John Pombe Magufuli kasema ununuzi wa meli mpya uko pale pale. Tutanunua meli ya kusafirisha abiria katika Ziwa Victoria kama ambavyo aliahidi wakati wa kampeni,” alisema huku akishangiliwa.

Ametoa kauli hiyo jana wakati akitoa maelekezo baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Kagera ambako amewasili leo kwa ziara ya siku tatu kwa ajili ya kukagua masuala ya wakimbizi pamoja na mwenendo wa ranchi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na jinsi zinavyotumika.

Mbali ya ununuzi wa meli hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali pia imejipanga kununua ndege mbili ili kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini. “Tuna dhamira ya kununua ndege walau mbili kwa ajili ya shirika letu la ndege la ATC. Tumelazimika kuwaomba Watanzania wenzetu warudi nyumbani ili kusaidia kuendesha shirika letu,” alisema.

Waziri Mkuu alisema suala hilo limeshafika mbali na utekelezaji wake hautachukua muda mrefu kuanzia sasa.

Alitumia fursa hiyo kuwaarifu wana Kagera kwamba hivi karibuni Serikali itaanza mradi wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta ambalo litapita kwenye mkoa huo na hivyo kutoa ajira kwa wakazi wake. “Bomba litaanzia Tanga, kupitia Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Geita, Kagera hadi Uganda. Na humu njiani litakuwa na vituo vya kusukumia mafuta, kwa hiyo tuna uhakika wa kupata ajira kwa ajili ya watu wetu,” alisema.