Wednesday , 16th Nov , 2016

Serikali imedhamiria kukamilisha na kuimarisha mtandao wa usafirishaji na usambazaji umeme nchini ili kufikia malengo ya dira ya taifa ya kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2025 ya kuhakikisha miji na vijiji vyote vya Tanzania vinakuwa na umeme.

Waziri Mkuu akipewa maelezo kuhusu mradi huo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua mradi wa kuboresha upatikanaji wa umeme   Jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amesema kuwa hadi sasa serikali imeshatenga shilingi trilioni  moja kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye vijiji elfu nane nchi nzima ili wananchi wanaoishi maeneo hayo waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi bila vikwazo.

Ameongeza kuwa kwa kutambua tatizo la wananchi wasiokuwa na uwezo wa kulipia fedha nyingi za kuvuta umeme hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini, serikali kupitia shirika la umeme Tanzania-TANESCO imepunguza bei ya kuvuta umeme kwa wananchi hao ambapo wametakiwa kuvuta umeme huo kwa shilingi elfu ishirini na saba tu.

Waziri Mkuu akiongoza uzinduzi wa mradi

Awali akimkaribisha waziri mkuu kuzindua mradi huo, Waziri wa Nishati na madini Mheshimiwa Sospeter Muhongo amelitaka shirika la umeme TANESCO kuhakikisha tatizo la mgao na ukatikaji wa mara kwa mara wa umeme katika jiji la Dar es salaam lisijitokeze tena.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Felchesmi Mramba amebainisha kuwa mradi uliozinduliwa leo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 70 ambapo umelenga kutoa umeme wa uhakika kwa wananchi wote wa jiji hilo huku ukiwa na lengo la kutatua changamoto ya kuelemewa kwa miundombinu ya umeme ambayo imekuwa ikizidiwa kutokana na ongezeko la mahitaji.