Tuesday , 31st May , 2016

Serikali ya Tanzania imetangaza kuanza kuimarisha Zahanati pamoja na hospitali za Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam ili kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na wanawake wanaokwenda kujifungua.

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli alipotembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa mara ya kwanza akiwa rais

Serikali ya Tanzania imetangaza kuanza kuimarisha Zahanati pamoja na hospitali za Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam ili kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na wanawake wanaokwenda kujifungua katika Zahanati na vituo hivyo hali itakayosaidia kuondokana na msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulusubisya wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi la hospitali hiyo ya taifa.

Msongamano mkubwa wa Wagonjwa katika Hospitali hiyo ya Taifa unachangiwa na ukosefu wa vifaa tiba pamoja na wataalam wabobevu katika Zahanati pamoja na vituo vya afya vilivyopo katika jiji la Dar es salaam.

Dkt .Mpoki Ulusubisya anasema mama wajawazito wanalazimika kufika katika Hospitali ya Taifa ili kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua kutokana na hali hiyo.

Dkt. Ulusubisya amesema kumekuwa na kiwango kikubwa cha ongezeko la watoto wanaozaliwa nchini hali inayohitaji elimu ya kutosha ya uzazi ili kuweza kuratibu huduma za afya nchini.

Hospitali za Rufaa nchini zilizopo katika kanda pia zinakabiliwa na uchache wa watumishi wa afya ikiwa ni pamoja na madaktari huku serikali ikiendelea kufanya jitihada za kuongeza watumishi.