Wito huo umetolewa na Mwanazuoni Adam Foya alipokuwa akiongea na East Africa Radio, na kuishauri serikali ijayo nini ifanye ili kuweza kumnufaisha kijana kwa kusimamia ukusanyaji wa kodi.
"Serikali ijayo ina jukumu kubwa la kuboresha mazingira ya ukusanyaji wa kodi, kuongeza kiwango na idadi ya walipa kodi, hata kama wanavyodai watapunguza baadhi ya kodi, ila wakiongeza idadi ya walipa kodi kwa kurasimisha biashara na kutengeneza mazingira rafiki, kutakuwa na kundi kubwa zaidi la walipa kodi, kwa hiyo hawataona machungu sababu kila mtu anatoa kwa sehemu kuliko ilivyo sasa hivi, ambapo wachache ndio wanaobeba mzigo mkubwa zaidi wa kulipa kodi", alisema Foya.
Foya ameendelea kusema kwamba kwa sasa vijana wengi wanafanya biashara isiyo rasmi, hivyo huipa serikali ugumu wa ukusanyaji wa kodi, na wakati mwengine kutoona umuhimu wa kulipa kodi kwa kuwa hakuna mazingira mazuri ya kuyakusanya.
"Kwenye suala la nani analipa kodi kumekuwepo na changamoto kubwa haswa kwenye kundi la vijana, vijana wengi wanajishughulisha kwenye shughuli ambazo zinaitwa sio rasmi kwa hiyo kodi za moja kwa moja walikuwa hawalipi, na wakati mwengine hawaona sababu ya kulipa kodi kwa sababu hakuna mazingira mazuri ya kuikusanya, vile vile hawaoni kodi yao ikifanya mambo ya maendeleo", alisema Foya.
Pia Mwanazuoni huyo amesema Watanzania wanatakiwa kujitambua kuwa wao ni walipa kodi, na kufuatilia matumizi ya kodi hiyo kuwa na sauti katika mapato na matumizi, kwani kwa kutofanya hivyo kutaleta matatizo katika mfumo wa ukusanyaji wa kodi.

