Monday , 5th Oct , 2015

Serikali imetakiwa kutoa kipaumbele katika masuala ya teknolojia, ili kuweza kukabiliana na maendeleo ya kisayansi na teknolojia yaliyopo, kwani mabadiliko ya sasa hivi ya dunia yanategemea teknolojia kwa kiasi kikubwa.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa baraza la vijana Fahimi Mastawili, alipokuwa akiongea kwa njia ya simu kwenye kipindi cha super mix kinachorushwa na East Africa radio.

Mastawili amesema Umuhimu wa teknolojia ni mkubwa sana kwa maisha ya sasa, hivyo serikali ina wajibu wa kuboresha sekta ya teknolojia, ili kuwaunganisha vijana pamoja kokote duniani, na kuwawezesha kujitengenezea fursa mbali mbali za ajira.

"Naiomba serikali ijayo, yoyote ile itakayoingia madarakani, kuweza kuwasaidia vijana kuwaunganisha pamoja, kwa maana kupata elimu kupitia teknolojia, kufanya uzalishaji na shughuli zozote zile kwa kiwango kikubwa sana, kwani madalikio sasa hivi yameingia kwenye matumizi makubwa ya teknoloji, sasa hivi watu wanatafuta ajira kwa kutumia teknolojia", alisema Mastawili.

Mastawili aliongeza kwa kusema kwamba lazima teknolojia iingizwe kwenye mitaala ya elimu, ili kuweza kuongeza elimu na uelewa wa matumizi ya teknolojia, hususan kwa vijana ambao wako vijijini ambao wana changamoto kubwa ya matumizi ya teknolojia.

Kwa upande mwengine Mastawili amesema iwapo serikali haitaboresha na kuinua sekta ya Teknolojia nchini, itakuwa imewanyima haki vijana wa tTanzania, ambao wana uhitaji mkubwa wa kutatua masuala yao.

"Niseme tu serikali ijayo itakuwa haitutendei haki vijana wa Tanzania ambao na sisi tutakuwa tumeshiriki kuichagua kuingia madarakani, na sisi ndio wengi katika nchi yetu, alafu bado suala la teknolojia isilipe kipaumbele kwa vijana kwa sababu itakuwa ni msaada mkubwa kwa vijana hawa ambao wanahangaika na kwa kiasi kikubwa wakiwa na matatizo ya afya, elimu ya afya kwa vijana, madawa ya kulevya, hivyo wako katika hali ya hatari sana", alisema Mastawili.