Sunday , 7th Sep , 2014

Mtaalam wa magonjwa ya saratani ya matiti kutoka hospital ya Aga Khan jijini Dar es salaam nchini Tanzania Dkt. Aidan Njau amesema tatizo la saratani ya matiti kwa wakina mama linaweza kutibika iwapo tu litawahiwa na kupatiwa matibabu mapema.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa zoezi la upimaji wa saratani ya matiti kwa wakina mama, Dkt. Njau amesema amewashauri wakina mama kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua tatizo mapema na kuweza kupata matibabu kabla ya tatizo hilo la saratani ya matiti halijasambaa katika mfumo wa damu.

Dkt. Njau amesema tatizo la ugonjwa wa saratani kwa kina mama hapa nchini bado ni kubwa hasa katika maeneo ya vijijini ambapo huduma za upimaji wa ugojwa huo zikiwa ni duni.

Kauli ya wataalamu hao wa tiba kutoka hospitali ya Aga Khan imekuja wakati ambapo Tanzania inakabiliwa na ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani kila mwaka licha ya hospitali zenye uwezo wa kubaini na kutoa tiba za ugonjwa huo kuwa chache.