
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa Nsola mkoani Mwanza
Makamu wa Rais ametoa maagiza hayo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika wilaya za Kwimba, Misungwi na Magu mkoani Mwanza katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Makamu wa Rais amewataka viongozi hao kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaokamatwa wakivua kwa zana haramu ua kwa sumu ili kukomesha tatizo hilo katika Ziwa Victoria.
Ameonya kuwa wavuvi haramu wakiachwa waendelee kufanya uvuvi huo wataharibu ziwa lote hasa mazalia ya samaki hali ambayo itasababisha viwanda wa kusindika samaki mkoani humo kufungwa na mamia ya watu kukosa ajira kutokana na shughuli za uvuvi.
Shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria
Akizindua na kuweka mawe ya msingi kweye mabweni ya wanafunzi wasichana katika shule za sekondari ya Idetemya wilayani Misungwi na shule ya Sekondari ya Archbishop Anthony Mayala wilayani Kwimba, Makamu wa Rais amepongeza juhudi za viongozi wa mkoa wa Mwanza na wadau wa maendeleo kwa kujenga mabweni hayo ambayo yatasaidia wasichana kuondokana na mazingira hatarishi ikiwemo kupata mimba.
Makamu wa Rais amewaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuweka mikakati madhubuti ya kujenga mabweni ya wasichana kama hatua ya kukabiliana na tatizo la wanafunzi kupata mimba na kuacha shule.
Akisalimia mamia ya wananchi wa maeneo ya Igoma na Nyakato jijini Mwanza waliojitokeza barabarani ili kumsalimia, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi hao kuwa ahadi zote zilizotolewa na viongozi hao wakati wa kampeni zitatekelezwa ikiwemo tatizo la ajira kwa vijana.
Amewahimiza wananchi waunge mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano katika kubaini wala rushwa na watendaji wanaohujumu miradi ya maendeleo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano inataka kuona rasilimali zilizopo nchini zinatumika vizuri kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote na sio kwa idadi ya watu wachache.
Makamu wa Rais akiwa katika shule ya Sekondari Idetemya, Misungwi Mwanza
Akiwa mkoani Mwanza Samia Suluhu Hassan amekagua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara na kuwaeleza mipango ya mikakati ya serikali ya awamu ya tano ya kuwaletea wananchi hao maendeleo.