
Zaidi ya wahamiaji haramu 117 waliingia nchini Tanzania kinyume cha sheria mwaka uliopita kupitia mkoani ya Rukwa, na kuufanya mkoa huo kuongoza kwa tatizo kubwa la wimbi la wahamiaji haramu nchini ambao wanatokea katika nchi za jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Zambia na zile za Rwanda na Somalia.
Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Rukwa Bw. Selemani Kameya amesema nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio iliyoongoza kwa kuwa na wahamiaji haramu 83 waliokamatwa, na kwamba operesheni maalumu iliyofanyika mwishoni mwa mwaka uliopita kwa kushirikiana na jeshi la polisi na viongozi wa vijiji mbalimbali ilifanikiwa kuwaondoa zaidi ya wahamiaji haramu 1,590 waliokuwa wakiishi nchini kinyemela.
Kwa upande wao baadhi ya maafisa wa uhamiaji wa mkoa wa Rukwa wakielezea juu ya utendaji wa kazi zao, wamesema wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri yakiwemo maboti yaendayo kwa kasi kutokana na jiografia ya mkoa wenyewe, na hivyo kuhitaji sana ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi kwa kuwafichua wahamiaji haramu badala ya kuwaficha.