Saturday , 24th Jan , 2015

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa pamoja na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo wamatakiwa kuondoka katika wilaya hiyo endapo watashindwa kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt Rajabu Rutengwe

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt Rajabu Rutengwe amekasirishwa na utendaji wa miradi ya maendeleo  wilayani Kilosa ikiwemo ujenzi wa vyumba vya maabara ambapo amemtaka mkurugenzi wa halmashauri Iddy  Mshiri na mkuu wa wilaya hiyo Eliasi Tarimo kufungasha virago na kuondoka endapo watashindwa kukamilisha maabara hizo ifikapo May 30 mwaka huu.

Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wakati akiendelea na ziara yake wilayani Kilosa ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi ambapo amesema hatakubali kuona viongozi hao wakishindwa kutekeleza agizo la Rais naye akakaa kimya badala yake wafungashe virago waondoke.

Awali akisoma taarifa ya wilaya kaimu mkuu wa wilaya ya Kilosa  hilary Sagara amesema wilaya inahitaji kuwa na vyumba 111 katika shule 37 za sekondari za serikali ambapo kwa sasa ina vyumba 15 pekee huku mkurugenzi mtendaji wa halimashauri hiyo Iddy Mshiri akimwahidi mkuu wa mkoa wa Morogoro Rajab Rutengwe watahakikisha kuwa kwa muda uliobakia  watamalizia maabara zote zinazohitajika

Katika hatua nyingine wananchi wa kijiji cha Mvumi wameomba mkuu huyo wa mkoa kushughulikia migogoro ya mipaka kati ya kijiji cha Mvumi na mgongoni ili kuepusha mgogoro mkubwa unaohatarisha uvunjifu wa amani kati ya vijiji hivyo vinavyo gombania mipaka ikiwa ni pamoja na kero ya mwekezaji ambaye anasababisha wananchi hao kukosa maeneo ya kulima hasa kipindi hiki cha kilimo.