Saturday , 25th Jun , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo, amezindua kituo cha mawasiliano cha Jeshi la Polisi ambacho kitarahisisha utoaji wa taarifa za uhalifu na kuharakisha askari polisi kufika katika eneo la tukio.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na baadhi ya viongozi wa jeshi hilo wakati wa ufunguzi wa kituo cha mawasiliano

Kituo hicho cha kwanza kuanzishwa na Jeshi la Polisi hapa nchini kipo katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kinafanya kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu na mfumo wa utambuzi wa eneo (GPS) ambapo askari polisi waliopo katika kituo cha mawasiliano watakuwa wakipokea simu kutoka kwa wananchi wanaotoa taarifa za matukio ya uhalifu na kisha kuwaelekeza askari walio jirani ili wafike eneo la tukio na kukabiliana na wahalifu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu amemueleza Rais Magufuli kuwa kituo hicho kina uwezo wa kupokea simu 18 kwa mpigo kutoka kwa watu wanaopiga simu ya bure namba 111 au 112 kwa ajili ya kutoa taarifa za uhalifu na kwamba lengo la jeshi hilo ni kuhakikisha askari wanafika eneo la tukio ndani ya dakika 15.

IGP Mangu ameongeza kuwa kituo hicho kimeanzishwa kwa msaada kutoka benki ya CRDB iliyotoa shilingi milioni 320, kitaanza kutoa huduma tarehe 01 Julai, 2016 kikianzia katika mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Kanda maalum ya Dar es Salaam na polisi imejiwekea malengo ya kuwa na vituo kama hivyo nchi nzima ifikapo mwaka 2019.

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuanzisha mradi huo na ameahidi kuwa serikali itahakikisha inaunga mkono mpango huo ikiwa ni pamoja na kulifanyia kazi ombi la kununuliwa helkopta itakayorahisisha zaidi ufikaji eneo la tukio.

Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi kuwanyang’anya silaha wahalifu kabla hawajawadhuru raia na kupora mali zao ama kusababisha mauaji, na amewataka viongozi wa jeshi hilo kuwazawadia askari wanaofanya kazi nzuri ya kupambana na wahalifu.

Dkt. Magufuli pia ametaka jeshi la polisi lisimame imara kuhakikisha serikali inatekeleza ahadi zake kwa wananchi zikiwemo upatikanaji wa maji na huduma nyingine za kijamii na kwamba hatarajii kuona mtu yeyote anafanya vitendo vitakavyosababisha ahadi hizo kutotekelezwa.

Katika hatua nyingine, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kuiongoza nchi.

Mufti Mkuu Sheikh Aboubakar Zubeir Ali ametoa pongezi hizo jana jioni tarehe 24 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam katika futari iliyoandaliwa na Rais Magufuli na akatumia nafasi hiyo kuwasihi Waislamu na watanzania wote kwa ujumla kukataa vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

“Niwahusie ndugu zangu watanzania wote, kwamba amani ni kitu muhimu tuitunze amani tuliyokuwa nayo, tuienzi amani tuliyonayo, na hapo tutakuwa tunaisadia serikali na tutakuwa tunamsadia Mhe. Rais katika kuilinda amani,” alisema Mufti Mkuu.