Sunday , 3rd Apr , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea kuwasisitizia watanzania wote kuendelea kuliombea taifa ili liendelee kuwa na amani na utulivu kwa maendeleo ya wote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

Rais Magufuli amesema hayo leo alipoungana na waumini wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, kusali ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka ambapo aliongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mhe. Raila Amoro Odinga na Mkewe Mama Ida Odinga.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye yupo mapumzikoni nyumbani kwake Lubambangwe katika kijiji cha Mlimani alitumia muda huo kuwaomba watanzania wote kuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja na siku zote kumtanguliza Mungu kwa kila Jambo.

“Wakati tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane" Amebainisha Rais Magufuli

Katika salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Mhe. Odinga amewashukuru watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na wakenya, huku akitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.

Mhe. Odinga ametoa mfano wake mwenyewe kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi ya kusafiria ya Tanzania, aliyoitumia kwa miaka mitatu kwa ajili ya kwenda kusoma nje ya nchi, baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya kukataa kumpa pasi hiyo.

Mhe. Odinga amemtaka Rais Magufuli kukabiliana na vikwazo vitakavyoibuka katika uongozi wake huku akimsisitizia kuendelea kumuomba mungu ili aweze kuongoza kwa uwazi, na haki kwa Watanzania wote.

Kuhusu urafiki wake na Rais Magufuli, Mheshimiwa Odinga amesema urafiki huo ulianza tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye kuwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya ujenzi wa barabara, na kwa umuhimu huo ametoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliojengwa na waasisi wake wakiongozwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Sauti ya Dkt. John Magufuli akisistiza kuliombea taifa
Sauti ya Raila Odinga akiongea kuhusu Rais Magufuli