Tuesday , 5th Jan , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wanne Ikulu Jijini Dar es salaam ambapo wamezungumzia mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wa Serikali ya awamu ya Tano.

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana baada ya kufanya mazungumzo na Prof. Mussa Juma Assad Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Akizungumzia yaliyojiri katika Mazungumzo hayo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Assad amesema wamezungumzia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Profesa Assad amebainisha kuwa Rais Magufuli ametaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ihakikishe Tanzania inaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya pato la Taifa (GDP) kwa mujibu wa hesabu zilizofanyika mwaka juzi.

"Hadi Mwaka juzi Tanzania ilikua inakusanya mapato kwa kiwango cha asilimia 14 ya pato la Taifa ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikua ikikusanya asilimia 19 ya pato Taifa, na hakuna sababu za Msingi za kwa nini Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo" aliongeza Profesa Assad.

Rais Magufuli pia amekutana na Mkurugenzi wa Mashitaka hapa Nchini (DPP) Mheshimiwa Biswalo Eutropius Mganga ambaye amesema mazungumzo yao yalijikita katika suala la kupeana mikakati ya namna ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka inavyopaswa kufanya kazi ili kuendana na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano isemayo "Hapa Kazi Tu"

Aidha Mganga ameongeza kuwa wamezungumzia umuhimu wa kuwahimiza watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yake itatekeleza wajibu wake bila kumuonea mtu.

Kiongozi Mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuber Ally ambaye pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake, amesema waislamu wote nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee na juhudi hizo.

"Na pia kwa niaba ya Waislamu tunataka kumueleza kwamba kazi anayoifanya ni kazi ambayo tunairidhia na tunamuomba aendelee kuifanya wala asiogope, na kauli yake ya Hapa Kazi Tu iendelee, kwa sababu inaonesha kwamba sasa nchi yetu itakaa mahali pazuri" Alibainisha Mufti Mkuu

Kiongozi Mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Alhaji Abdallah Majura Bulembo ambaye amempongeza Mheshimiwa Rais kwa kasi nzuri aliyoanza nayo katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015- 2020 na kutaka kasi hiyo iendelee.

Amesema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli na kwamba Mheshimiwa Rais amemuhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo zaidi katika kutekeleza Ilani ya CCM.

"Tunafurahi kwamba yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa ada za shule, na hivi sasa wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada" alisisitiza Alhaji Bulembo