Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wahitimu wakati alipokuwa Mgeni rasmi katika Mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika chuoni Bingo kibaha Mkoani Pwani aliyeketi kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho Mizengo Peter Pinda Novemba 24,2016
Rais Magufuli Magufuli ametoa kauli hiyo leo 2016 katika sherehe za mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania zilizofanyika Bungo, Kibaha Mkoani Pwani.
Katika hotuba yake Rais Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za Serikali ambao wamekuwa wakitumia vibaya fedha za umma ikiwemo kuweka fedha nyingi za Serikali katika akaunti za muda maalum (Fixed Deposit Account) kwenye benki za biashara ambako hujipatia fedha kupitia faida ya akiba bila kujali kuwa vitendo hivyo husababisha Serikali kukosa fedha na kulazimika kukopa kutoka benki za biashara ambako hutozwa riba kubwa.
Rais Dkt John Magufuli
"Sasa sifahamu kama Chuo Kikuu Huria na nyinyi mmekuwa mkiweka fedha za maendeleo katika Fixed Deposit Account, lakini huo ndio umekuwa ni mchezo, juzi hapa tumekuta fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 26 zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye benki tatu kama Fixed Deposit Account na Bodi ya TRA ikapitisha, ndio maana nilipozipata hizo taarifa, fedha nikachukua na Bodi kwa heri.
"Hata kwa sasa hivi Waziri upo hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ilianzishwa kwa sababu maalum, inachangiwa fedha wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye Fixed Deposit Account, Waziri hiyo ni message sent and Delivered" amesisitiza Rais Magufuli.
Mkuu wa Chuo hicho Mizengo Peter Pinda akitunuku Shahada, Stashahada na Vyeti mbalimbali vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika Mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu hicho yaliyofanyika chuoni Bingo kibaha Mkoani Pwani Novemba 24,2016
Katika Mahafali hayo, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amewatunuku shahada na vyeti jumla ya wahitimu 4038, wakiwemo wahitimu 8 wa shahada ya Uzamivu, 217 wa shahada ya Uzamili, 111 wa Stashahada ya Uzamili, 1,186 wa Shahada ya Kwanza, 484 wa Stashahada na 1,421 wa vyeti mbalimbali.