Kivuko kinachotumika kuvusha watu na magari katika mto Kilombero
Historia imeandikwa jioni ya jana, Jumatano, Agosti 20, 2014 katika Mkoa wa Morogoro na katika Tanzania. Kwa mara ya kwanza tokea enzi na enzi, magari yameweza kuvuka Mto wa Kilombero, moja ya mito mikubwa zaidi nchini, mpakani mwa Wilaya za Ulanga na Kilombero katika Mkoa wa Morogoro.
Magari hayo ya msafara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yamevuka Mto Kilombero kwa kutumia daraja dogo la muda ambalo wajenzi wa daraja kwenye mto huo wamelijenga kwa ajili ya kurahisisha kazi yao ya ujenzi wa daraja hilo kubwa. Daraja hilo la muda la chuma lina uwezo wa kubeba tani 100.
Rais Kikwete na msafara wake wa magari kiasi ya 20 umevuka Mto Kilombero kwa kutumia magari ukitokea Wilaya ya Ulanga kuingia katika Wilaya ya Kilombero kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo katika sherehe iliyofanyika upande wa mto wa Wilaya ya Kilombero, kilomita kiasi cha saba unusu kutoka mjini Ifakara.
Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero kwenye siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku saba katika Mkoa wa Morogoro.
Rais Kikwete ameanzia ziara hiyo katika Kijiji cha Mwaya ambako amezindua Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini na pia kuzindua Mradi wa Mfumo wa Huduma za Afya za Masafa (Telemedicine).
Daraja hilo linalojengwa kwenye Mto Kilombero unakamilisha ujenzi wa madaraja matano makubwa nchini ambayo yalikuwa yamepangwa kujengwa katika Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo mwaka wa fedha wa 1967-1968 lakini likashindikana kujengwa kwa miaka 47 iliyopita mpaka sasa.
Daraja hilo linalogharimu Sh. bilioni 55.8 ambazo zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania linajengwa na Kampuni ya China Railway 15 ya China, lina madaraja mawili – kubwa ambalo lina urefu wa mita 384 na dogo lenye urefu wa mita 120, litakuwa pia na makaravati 35, na njia ya watu kupita kwa mguu na baiskeli.
Daraja hilo lenye uwezo wa kubeba tani 180 kwa wakati mmoja, pia litajengwa pamoja na barabara ya lami ya kilomita 9.5, ikiwa ni kilomita saba unusu upande wa Ifakara na kilomita mbili upande wa Wilaya ya Ulanga.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo iliyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi pamoja na kwamba Rais Kikwete alikawia kidogo kufika darajani hapo kwa sababu ya shughuli za uzinduzi wa miradi mingi kwenye Wilaya ya Ulanga, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick Mufugale amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo umechelewa kidogo kwa sababu ya tuta na daraja la mwanzo la muda kuchukuliwa na maji wakati wa mafuriko ya mwaka huu.
Amesema kuwa kutokana na tukio hilo, ujenzi wa sasa umefanyiwa marekebisho makubwa ambayo yataliwezesha tuta la sasa kuweza kuhimili aina yoyote ya mafuriko makubwa hata kwa miaka 100 ijayo.
Baada ya kushindikana kujengwa kwa miaka mingi, Rais Kikwete, wakati akiwa Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 aliahidi ujenzi wa daraja hilo. Aidha, ujenzi huo uliwekwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo na kupanda Mti wa Kumbukumbu, Rais alikumbusha historia ya ujenzi wa daraja hilo akisema kuwa katika Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo, Serikali iliamua kujenga madaraja matano makubwa nchini.
Amesema kuwa madaraja hayo ni Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Daraja la Mto Rufiji, Daraja la Kigamboni, Dar Es Salaam; Daraja la Mto Kilombero na Daraja la Mto Malagarasi.
Amesema kuwa kati ya madaraja hayo, Uongozi wa Awamu ya Kwanza ulijenga Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara na Uongozi wa Awamu ya Tatu ukajenga darala la Mto Rufiji.
“Sisi tuliamua kujenga madaraja matatu makubwa – Kigamboni na kwenye Mito Malagarasi na Kilombero. Lile la Malagarasi limekamilika, lile la Kigamboni linakamilika na litakuwa tayari Juni, mwakani, wakati leo tumeweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa hili la Kilombero ambalo ujenzi wake tayari umeanza.”
Rais Kikwete ambaye ameanza ziara ya Mkoa wa Morogoro leo, kesho ataendelea na ziara yake katika Wilaya za Morogoro