Wednesday , 24th Jul , 2019

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amemfukuza kazi aliyekuwa Waziri wa Fedha, Henry Rotich ikiwa ni siku moja tu baada ya Rotich, kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za ufisadi, ambapo Waziri wa Kazi, Ukur Yattani ameteuliwa kukaimu nafasi hiyo.

Rotich alifika Mahakamani jana Julai 23, ikiwa ni siku moja tu baada ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) nchini Kenya Noordin Haji, kuagiza Waziri huyo wa fedha pamoja na maafisa wengine  washtakiwe kwa ufisadi.

Waziri huyo aliwasili mahakamani hapo akiwa na wenzako na kisha aliachiwa huru kwa dhamana ya  $150,000, baada ya kukana zaidi ya mashtaka 10 yanayohusiana na ufisadi, ambapo Rotich, na mshtakiwa mwenzake, Katibu Mkuu Kamau Thugge waliagizwa kuwasilisha pasipoti zao za usafiri kama sehemu ya masharti ya dhamana.

Ambapo Hakimu Douglas Ogoti, aliwazuia kutofika katika Makao ya wizara ya fedha na kufafanua kwamba eneo hilo linachunguzwa kwa uhalifu.

Rotich alikanusha mashtaka ya ufisadi dhidi yake, kuhusiana na kandarasi ya ujenzi wa mabwawa mawili, siku moja tu baada ya kukamatwa na kuzuiliwa.