Wednesday , 23rd Dec , 2015

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na spika wa seneti na mjumbe maalum wa Rais wa jamhuri ya Burundi mhe. Reverien Ndikuriyo ikulu jijini Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Ndugu Reverien Ndikuriyo Spika wa Seneti wa Bunge la Burundi.

Rais Magufuli amesema suala kubwa waliloongelea ni kuhusu hali ya Kisiasa na usalama nchini Burundi na jitihada zinazochukuliwa na Tanzania ikiwa ni mwenyekiti wa jumuia ya Afrika Mashariki.

Akiwasilisha ujumbe wa Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi kuhusu hali ya Burundi, Spika Ndikuriyo amesema serikali ya Burundi ipo tayari kufanya mazungumzo na wadau wote wa siasa kuhusu hali ya Burundi na jitihada za kuumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Akitoa maelezo ya kikao hicho kwa niaba ya Rais Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Augustine Mahiga amesema serikali ya Burundi imekubali usuluhishi unaofanywa na Rais wa Uganda mh. Yoweri Kaguta Museveni kwa niaba ya marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Balozi Mahiga amesema Burundi inaamini kuwa hakuna hali ama dalili za kutokea kwa mauaji ya kimbari kama ya Rwanda, na Kwamba kwa sasa kuna utulivu nchini humo tofauti na wasiwasi wa Umoja wa Ufrika, jumuiya za kimataifa hasa Umoja wa Ulaya.