Wednesday , 9th Jan , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro kufuatia askari wake kuhusika na tuhuma za kudai rushwa pindi walipowakamata waharifu wa madini.

Rais Dkt John Pombe Magufuli

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam wakati akiwaapisha Mawaziri wawili pamoja na makatibu wa wizara mbalimbali ambapo aliahidi kuendelea kufanya mabadiliko mara kwa mara pindi atakapokuwa hajaridhika na utendaji kazi.

Rais Magufuli amesema, "nampongeza IGP kwa kushughulikia suala la madini kule Mwanza, umefanya kazi nzuri, umefanya vyema kuwakamata wale Askari waliokuwa wakizungumza na mtuhumiwa ili wapewe rushwa, na walishapewa milioni 700 na nyingine waliambiwa watapewa Sengerema".

Aidha Rais Magufuli amesema, "askari wa Polisi waliendelea kuzunguka na watuhumiwa wa madini kwa kutumia magari na mafuta ya Serikali, niliwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema ili wakamatwe, iliwekwa road block na wakakamatwa".

Miongoni mwa Mawaziri ambao walioapishwa na Rais Magufuli ni Waziri wa ofisi ya Waziri Mkuu na Uwekezaji Angela Kairuki, na pamoja na Waziri wa Madini Dotto Biteko.