Bi. Sakaya ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio na kusema kwamba endapo Rais Magufuli atatekeleza hilo, watanzania watapata manufaa.
"Rais amchague waziri kwa kujua waziri huyu atafanya kazi vizuri, atakuwa mtumishi wa watanzania, nakuthibitishia ndani ya miaka miwili nchi hii itakuwa vizuri, kwa kuwa yeye mwenyewe atasimamia vizuri, kila waziri atakuwa active, makatibu wote watakuwa active, bunge litakuwa active, tutakwenda vizuri, Watanzania watapata manufaa", alisema Magdalena Sakaya.
Mbunge huyo aliendelea kwa kusema kwamba endapo Rais hatakuwa na mbia kwenye urais wake, atafanya kazi vizuri na kumtaka kuteua mawaziri nje ya bunge iwapo mtu anafaa kwa nafasi hiyo.
"Kama hatakubali kumezwa akasimama kama Rais, asiwe na mbia na urais wake, atafanya kazi vizuri, ateue mawaziri hata nje ya bunge, maadam ni mchapa kazi, awalete awaapishe wafanye kazi", alisema Magdalena Sakaya.
Pamoja na hayo Bi Sakaya ameelezea imani yake kwa Rais Magufuli, na kuwataka wananchi kuwa na imani na Bunge la awamu hii kuwa litafanya kazi ya kuwawakilisha wananchi ipasavyo.
"Mimi nina imani binafsi kwamba Bunge ambalo tutakuwa nalo kipindi hiki, Rais atatengeneza baraza zuri, akapata waziri mkuu mtenda kazi, anamchagua waziri sio kwa kushinikizwa na mtu, wala undugu wala rafiki", alisema Magdalena Sakaya.