Wednesday , 13th Jul , 2016

Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa amesema kwamba suala la ulinzi na usalama katika mkoa wa Dodoma linaendelea kufanyiwa kazi kama kawaida ya jeshi la polisi kufanya kazi hiyo mahali popote.

Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa

Kamanda Mambosasa ameyasema hayo mara baada ya kuwepo kwa taarifa za watanzania wanaoingia katika mji wa Dodoma kupekuliwa na kuhojiwa kuhusu mambo wanayokwenda kufanya katika mkoa huo.

Akielezea swala hilo katika kipindi cha EA DRIVE Kamanda huyo amesema wao hawana shida na mtu ambaye haashirii uvunjifu wa amani lakini BAVICHA walisema wanakwenda Dodoma ndiyo wanawatafuta na lengo lao ni jema la kuimarisha ulinzi katika mkoa huo.

''Ukaguzi tunafanya kweli katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba za kulala wageni na hili si jambo geni ni jambo ambalo linafanyika ili kuhakikisha amani inakuwepo.'' Amesema Kamanda Mambosasa

Aidha amesisitiza kwamba mtanzania ana haki ya kusafiri katika eneo lolote ndani ya nchi ila ahakikishe havunji sheria za nchi.

Tarehe 23 Julai chama tawala kinatarajia kufanya mkutano wake mkuu utakaopelekea kuchaguliwa kwa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.