Thursday , 24th Dec , 2015

Polisi wawili wa kituo kikuu cha polisi jijini Mwanza, wamefariki dunia baada ya mmoja wao kumpiga risasi ya bega askari mwenzake kisha naye kujipiga risasi chini ya kidevu na kutokea kichwani na kupelekea umauti.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Justus Kamugisha.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Justus Kamugisha, alisema mauaji hayo yalitokea jana saa 8:30 mchana katika mtaa wa barabara ya Pamba baada ya mmoja aliyekuwa kwenye lindo benki ya Posta kuamua ‘kukoki’ risasi na kumfyatulia mwenzake.

“Askari namba H5950 PC Petro Matiko alienda katika benki hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya kibenki kisha kuwakuta wenzake wawili wakiwa lindoni ambao ni H852 PC Masunga Elisha na H4291 PC Lemigius Alofoustin, kabla ya Matiko kutoka nje na kuwaeleza mtandao wa kibenki unasumbua,” alisema kamanda Kamugisha.

Kamugisha alisema baada ya Matiko kutoka ndani ya benki hiyo na kuwaeleza kuhusu kusumbua kwa mtandao, ghafla PC Elisha ‘alikoki’ bunduki yake huku mwenzake PC Alofoustin akimuuliza anachofanya ni hatari, lakini ghafla alimlenga Matiko bega la kushoto na kuanguka papo hapo.

Kamanda Kamugisha alisema baada ya Pc Matiko kuanguka chini, naye Pc Elisha alijilenga na bunduki chini ya kidevu na kujipiga risasi ilifumua kichwa chake huku mwenzake Pc Alofoustin akitoka mbio.

Hata hivyo, kamanda Kamugisha alisema Pc Elisha hakuwa na tatizo lolote tangu alipoanza kazi katika jeshi hilo, huku jeshi hilo likiendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo la mauaji.

Baadhi ya mashuhuda akiwamo Paulo Masanja, alisema alisikia mlio wa risasi ukitokea maeneo hayo ya benki wakati akiwa anasubiri kupanda daladala katika kituo cha Posta huku askari mmoja aliyevaa sare akitimua mbio.