
Akiongea na East Africa Radio leo ofisini kwake ambapo alikuwa akipokea watu mbalimbali waliokwenda kujifunza mambo yahusuyo siasa, Msajili msaidizi wa vyama vya siasa upande wa gharama za uchaguzi na elimu kwa umma Bi. Piencia Kiure amesema kuwa ni vyama vitatu pekee vilivyorudisha ripoti hiyo kati ya vyama 18 vilivyoshiriki uchaguzi mwaka 2015.
Akivitaja vyama ambavyo vimeshafanikiwa kurudisha ripoti hiyo mpaka hivi sasa ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), ACT Wazalendo na Chama cha Wananchi( CUF ) na siku ya mwisho ya kurudisha ripoti hizo ni hapo kesho.
Akifafanua adhabu kwa chama kitakachoshindwa kurudisha ripoti hiyo kwa wakati amesema kuwa ni faini isiyozidi shilingi milioni 3 au mgombea alieshindwa kurudisha ripoti kwa chama chake ni faini isiyozidi milioni 2 au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.