Mabaki ya miongoni mwanyumba zilizochomwa
Jumla ya kaya 366 hazina mahala pa kuishi baada ya nyumba zao zipatazo 785 ambazo zinaitwa mabanda, pamoja na mabanda ya tumbaku 118, kuchomwa moto na magunia zaidi ya 600 kuteketezwa,katika kile kilichodaiwa kuwa walikuwa wakiishi ndani ya hifadhi za Usoke, Igombe na Ugala, wilayani Urambo mkoani Tabora kinyume cha sheria.
Wakizungumza kwa masikitiko walipohifadhiwa na wananchi katika kijiji cha Kangeme, baada ya kuteketezwa kwa vyakula vyao mbalimbali vikiwemo uwele viazi na mahindi, ambayo yameishavunwa na mengine yakiwa shambani tayari kuvunwa huku wakilalamikia mengine kupolwa.
Mamia ya wananchi hao ambao wanadaiwa kuwa ni wavamizi wa hifadhi, pamoja na kukiri kuwepo ndani ya hifadhi ya Usoke, Igombe Ugala, wamelalamikia kukumbwa na janga la njaa, ambapo walikuwa wamepewa muda wa kuondoka ifikapo 31 Julai baada ya kuvunwa chakula chao.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Urambo ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kaliua, Bw. Saveli Maketa, aliyeambatana na uongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) amesema kuwa, kabla ya kuanza zoezi hilo aliwaonya watendaji hao kutokiuka haki za binadamu ambapo amesema kuwa, kuchoma chakula ambacho kipo tayari kwa matumizi ya binadamu ni sawa na mauaji.
Aidha mkuu wa mkoa wa Tabora Bi Fatuma Mwassa, amesema kuwa, uongozi wa mkoa ulitoa muda hadi tarehe 31 Julai ili kuondoa chakula chao huku akishangazwa jinsi hatua hiyo ilivyochukuliwa, akilalamikia kuchoma chakula ambapo ameunda tume ya uchunguzi ili kubaini uharali wa tukio hilo, ambapo mtendaji wa kijiji alishuhudia zaidi ya gunia 500 zikichomwa.