Tuesday , 10th Nov , 2015

Mkoa wa Njombe wanatarajia kuwa wenyeji wa maadhimisho wiki ya usafi wa mazingira na uchimbaji choo ambapo kitaifa yatafanyika mkoani humo na kufanyika kwa maonesho mbalimbali ya usafi wa mazingira na uboreshaji wa vyoo.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sarah Dumba akipanda mti ikiwa ni ishara ya upandaji miti na Utunzaji wa Mazingira Mkoani Njombe

Akizungumza na East Africa Radio afisa afya mkoa wa Njombe Mathias Gambishi amesema kuwa katika halmashauri zote mkoa wa Njombe zinatimiza kampeni za usafi wa mazingira na uboreshaji wa vyoo na kufanya maonyesho ya wiki ya usafi wa mazingira.

Amesema kuwa katika wiki hiyo kututakuwa na maonyesho mbalimbali ya usafi wa mazingira, unawaji wa mikono, utumiaji bora wa Choo pamoja na uchimbaji wa vyoo.

Amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuwa na vyoo bora na kutumia maji safi katika unawaji wa mikono kwa sabuni ili kuhakikisha kuwa anamaliza usafi bila kuondoka na uchafu.

Amesema kuwa idara ya afya mkoani humo inapata changamoto mbalimbali za kuhakikisha kuwa inawafikia wananchi moja kwa moja wakati wa kampeni za afya na usafi wa mazingira ambapo mkoa na halmashauri zote zinaendesha kampeni hizo.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yamepelekwa katika mkoa huo kutokana na mkoa huo halmashauri zake kufanya vizuri katika usafi wa mazingira kitaifa.