
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akiongea na vyombo vya habari katika mdahalo wa wahariri wa vyombo vya habari kuhusiana masuala ya ukeketaji,mimba na ndoa za utotoni.
Dkt. Ndugulile amesema kufuatia jamii hizo kubadili mwenendo wa ukeketaji na serikali kubaini mbinu hizo amesisitiza agizo lake alilolitoa mwaka jana, wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Mtoto wa Kike yaliyofanyika Mkoani Arusha la kuwataka madaktari wote nchini kufanya uchunguzi kwa watoto wote wachanga ili kubaini kama watoto hao wamefanyiwa ukatili kwa kukeketwa ili wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
"Takribani asilimia 37 ya wasichana nchini wanaolewa kabla ya miaka 18 wapelekeni wasichana shuleni kwani kadri msichana anavyokaa shuleni ndivyo anapunguza uwezekano wa kupata watoto na kuolewa mapema lakini pia elimu inamuwezesha kupata pato la uhakika", amesema Dkt. Ndugulile.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2018, takwimu za mimba za utotoni bado ziko juu Nchini huku mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni ni Katavi 45%, Tabora%, Morogoro 39%,Dodoma 39%, na Shinyanga 34%.
Mdahalo huo umefanyika wakati Tanzania ikielekea kuungana na nchi nyingine duniani, katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Oktoba 11, kufuatia agizo la Umoja wa Mataifa la mwezi Desemba mwaka 2011 la kuzitaka Nchi wanachama wa Umoja huo kuadhimisha siku hiyo ili kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukatili, ambapo kwa mwaka 2018 yatafanyika jijini Dar es salaam kitaifa.