Monday , 7th Sep , 2015

Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Mh. John Pombe Magufuli amesema kuwa serikali yake itatilia mkazo swala la ukusanyaji wa kodi hasa kwa wawekezaji wa nje na kuangalia upya misamaha ya kodi ili serikali kukusanya fedha nyingi zaidi.

Mgombea Uraisi kupitia chama cha Mapinduzi CCM, Mh. John Pombe Magufuli ikihutubia maelfu ya Wananchi Mkoani Morogoro

Mh. Magufuli ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara wakati wa kunadi sera zake katika uwaja wa Jamhuri mkoani Morogoro ambapo ameipongeza serikali ya Kikwete kwa kuongeza mapato lakini serikali yake itatilia mkazo zaidi katika suala hilo.

Dkt. Magufuli amesema kuwa wakati serikali ya Jakaya Kikete inaingia ilikuta ukusanyaji wa mapato ni bilioni 300 kwa mwezi na kupandisha mpaka bilioni 900 lakini serikali yake itataka kufikisha mara mbili ya hapo.

Katika hatua nyingine Magufuli amesema kuwa baraza lake la mawaziri atakaloliunda endapo atapewa dhamana na wananchi kuingia madarakani litakuwa la wachapa kazi na litakaloshughulikia kero za wananchi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema Tanzania ya sasa inahitaji kiongozi kama magufuli kwa kuwa imetoka kuongozwa na kiongozi mpole sasa inahitaji kiongozi mkali kuliongoza taifa.