Thursday , 31st Dec , 2015

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, amesema serikali yake iko tayari kuzungumza na wanamgambo wa Boko Haram ili kuwaachia huru wanafunzi wa kike 209 waliowateka nyara mwezi Aprili 2014, kwenye mji wa Chibok.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Buhari amesema wamejiandaa kuzungumza na Boko Haram ili kuwaachia huru wasichana hao waliotekwa mwaka uliopita kwenye mji huo wa kaskazini mashariki, kitendo kilichozuwa lawama kali ulimwenguni na wito wa kuachiwa kwao.

''Bado tumeweka wazi msimamo wetu kwamba kama Boko Haram watatuonyesha uongozi wenye kuaminika na wanatuambia wasichana wale wako wapi, basi tumejiandaa kuzungumza nao bila ya masharti yoyote ya awali,'' alisema Buhari.

Buhari amesema hakuna taarifa za kijasusi kuhusu mahali waliko wasichana hao, wala namna afya zao zilivyo na hivyo mazungumzo hayo yanaweza yakaanza tu iwapo maafisa wa Nigeria watathibitisha kuwa wasichana hao wako hai. Ameongeza kusema kuwa wanataka kupata uhakika kwamba wasichana hao wako salama.

Wanafunzi wa kike 276 walitekwa nyara na Boko Haram, lakini wasichana kadhaa walifanikiwa kutoroka muda mfupi baada ya kutekwa. Hata hivyo kiasi ya wasichana 200 hawajulikani walipo na hawajaonekana tangu video yao ilipoonyeshwa mwezi Mei mwaka 2014.