Monday , 25th Sep , 2017

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema atalishitaki Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kuingilia majukumu yake ya kikazi pale anapokuwa akitimiza wajibu wake wa kibunge ikiwa pamoja na kuzungumza na wananchi.

Mchungaji Msigwa amesema atakata rufaa kwa sababu polisi wamezuia mikutano yake miwili iliyokuwa ifanyike siku ya leo Juma tatu na kesho ambayo alitarajia kufanya katika kata za Kihesa na Kitwiru kwa madai ya kukiuka masharti alipohutubia katika Kata ya Mlandege.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Mchungaji Msigwa amesema chombo pekee kinachoweza kumtia hatiani  kwa kufanya uchochezi ni mahakama na sio polisi.

“Jana walinikamata tangu saa 11:30 na kuanza kunihoji mpaka saa 3:15 usiku kwa tuhuma za kufanya uchochezi lakini mimi nakakataa sijafanya uchochezi kwa sababau hakuna mtu anaweza kunizuia  kuongea na wananchi wangu, wanadai nimeleta hofu na kuvichonganisha vyombo vya dola na wananchi,” amesema Msigwa .

Mh. Msigwa ameongeza kwamba “Mimi niko tayari hata kama wangeniweka ndani wiki mbili siogopi kwa sababu sitanyamaza nitaendelea kuongea na sitaacha kusema kilichomtokea Tundu Lissu na ili kuninyamazisha ni lazima waniue kwa sababu nimeshajiandaa kisaikolojia,” amesema Mchungaji Msigwa.

Akizungumzia hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi amesema walimkamata Msigwa kwa kuwa alikuwa anatoa maneno ya uchochezi kwa wananchi aliokuwa anawahutubia mkutano wa hadhara Kata ya Mlandege na kuongeza kuwa  jeshi hilo linaendela na upelelezi juu ya tuhuma hizo na mara utakapokamilika watamfikisha mahakamani. 

Aidha Mchungaji Peter Msigwa amesema mpaka muda huu yupo nje kwa dhamana.