Tuesday , 5th Sep , 2017

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema Serikali haikupandisha mishahara kutokana na sakata la watumishi hewa na vyeti feki ambalo mchakato wake sasa umekwisha.

Katika kikao cha kwanza cha bunge kilichoanza leo, Mh. Angellah Kairuki amekiri kuwa mishahara pamoja na madaraja hayakupandishwa kwa sababu serikali ilikuwa inataka kufahamu namba sahihi ya watumishi ikiwa ni pamoja na kuangalia jinsi hali ya uchumi ilivyo.

“Tayari Serikali imeshatenga Sh600 bilioni kwa ajili ya kuanza kupandisha madaraja wafanyakazi wote ambao wanastahili. Na mishahara nayo itaongezwa kwa kadiri ilivyopangwa. Nikiri kweli hatukufanya zoezi hilo kutokana kuwa watumishi hewa walikuwa ni wengi na laiti tusingefanya zoezi hilo tungepoteza mabilioni ambayo yangepaswa kufanya kazi zingine.” amesema.

Kairuki alikuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Susan Masele  ambaye pia ametaka kujua kuhusu idadi ya vibali vya ajira vilivyotolewa na Serikali.

Waziri amesema Serikali imeshasaini vibali 10,000 kwa ajili ya kutoa ajira na vingine 4,000 viko mbioni kusainiwa.

Amesema sehemu itakayoangaliwa kwanza katika kuajiri ni nafasi za walimu na idara ya afya ambazo ndizo zilionekana kuathiriwa zaidi na vyeti feki.

Pamoja na hayo Mhe. Kairuki amekanusha uvumi kuwa serikali imeshindwa kuajiri kutokana na kukosa pesa.