Monday , 27th Oct , 2014

Baraza la Mitihani nchini Tanzania (NECTA) limewatahadharisha waajiri hapa nchini juu ya kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaotumia vyeti bandia kuomba ajira na kuwataka waajiri kupeleka vyeti vya watu wanaotaka kuwaajiri ili kuvikiki vyeti vyao.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini Tanzania, Dkt Charles Msonde.

Akiongea na waandishi wa habari leo, Meneja wa Fedha na Utawala wa (NECTA) Bw. Daniel Mafie ameelezea jinsi ambavyo tasisi hiyo inavyopambana na watu wanaotumia vyeti bandia katika kuombea kazi au masomo.

Aidha, NECTA imesema imeanzisha utaratibu wa kutoa vyeti mbadala kwa watahiniwa waliopoteza au kuunguliwa na vyeti vyao ili kuondoa mgogoro wa ununuaji wa vyeti bandia baada ya watu kupoteza vyeti.

Akifafanunua Mafie amesema kuwa katika mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2013 watahimiwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 13 tu ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliobainika kufanya udanganyifu mwaka 2011.

Aidha Mafie aliongeza kuwa katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2013 watahimiwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 272 ikilinganishwa na watahimiwa 789 mwaka 2012 na 3,303 mwaka 2011.

Akieleza zaidi kuhusu mafanikio yaliyofikiwa Mafie alisema Baraza hilo limeweza kusanifu mifumo ya Kompyuta yenye uwezo wa kupanga shule katika makundi ya ubora wa ufaulu katika matokeo ya mitihani ya Taifa.

Katika kukabiliana na tatizo la watu wanaotumia vyeti vya watu wengine au kughushi vyeti wakati wa kuomba ajira au nafasi za masomo katika shule mbalimbali ambapo kuanzia mwaka 2008/2009 Baraza hilo lilianzisha utaratibu wa kuweka picha za watahimiwa katika vyeti vyao.

Katika utaratibu huo vyeti hivyo viliwekewa alama za kiusalam hali ambayo imesaidia Baraza hilo kuwa na uwezo wa kubaini kwa haraka na kuwachukulia hatua wale wanaoghushi vyeti au kutumia vyeti vya watu wengine.

Baraza la Mitihani la Tanzania ni Taasisi ya Umma iliyochini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 21 ya mwaka 1973 na marekebisho yake ya mwaka 1998 na 2002 kwa ajili ya kuendesha mitihani ya Taifa kwa lengo la kuweka misingi ya sera ya mitihani, kuendesha mitihani na kutunuku stashahada mbalimbali na vyeti kwa watahiniwa wanaofuzu na kufaulu mitihani iliyo chini yake kisheria.

Katika hatua nyingine, chama cha siasa cha Alliance For Change and Transparency (ACT) nchini Tanzania kimesema hakikubaliana na Katiba iliyopendekezwa na hivyo kimetangaza kwenda mikoa mbali mbali hapa nchini ili kuwaeleza wananchi waipinge Katiba hiyo wakati wa kura ya maoni.

Katibu Mkuu wa ACT Bw. Samson Mwigamba, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati chama hicho kilipokuwa kikitoa maazimio ya mkutano mkuu wa tatu wa kamati kuu ya chama, uliofanyika Jijini Dar es Salaam Oktoba 25 mwaka huu.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa ACT amesema kamati kuu ya chama hicho imeridhia chama hicho kuwa kishiriki kwa nguvu zote katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Disemba mwaka huu.