Wednesday , 9th Jul , 2014

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) leo imekutana na vyama vya siasa kuzungumzia mchakato wa uchaguzi na maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura.

Jaji mstaafu Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania - NEC.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha kwamba wale wote wenye sifa za kupiga kura wanajitokeza kwa wingi na ndio maana wameamua kukutana na vyama vya siasa kwa kuwa wao ndio wadau wakubwa wa wapiga kura.

Amesema tume hiyo inatarajia kuanza maboresho ya daftari hilo kuanzia mwezi wa tisa kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki (BVR) ambapo wananchi wote wenye sifa na wale wenye vitambulisho vya kupigia kura watatakiwa kujiandikisha upya.

Aidha, vyama vya upinzani vimehoji ni wapi NEC itapata zaidi ya shilingi bilioni mia mbili inazotaka kutumia kwa ajili ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura wakati fedha zilizotengwa na bunge kwa ajili ya taasisi hiyo hazizidi shilingi bilioni saba.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuhudhuria mkutano na tume ya taifa ya uchaguzi, mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba amesema inashangaza kuona NEC inapanga matumizi ya kiasi kikubwa cha pesa huku ikijua kuwa bajeti iliyonayo haizidi asilimia moja ya gharama ya mradi mzima.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa chama cha mapinduzi CCM Abdulrahman Kinana amesema kulikuwa na haja ya kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za zoezi hilo hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia na mashine wanazotaka kutumia zinatumiwa pia katika zoezi la vitambulisho vya taifa.