Friday , 24th Aug , 2018

Pengine unaweza ukawa umezoea kupoteza simu na kutofuatilia zaidi tu ya kurejesha 'SIM card' yako kisha kununua simu nyingine, kitu ambacho si sahihi kwa mujibu wa sheria na unaweza ukaingia kwenye matatizo.

Kupitia kipindi cha East Africa Drive cha East Africa Radio kipengele cha 'GUTUKA', dada mmoja mkazi wa Dar es salaam ambaye hajataka jina lake kutajwa, ameeleza jinsi ambavyo alipoteza simu mwaka 2016 lakini amekuja kuipata mwaka 2018.

Ameeleza namna ambavyo aliipata ni kufuata utaratibu baada ya kupoteza simu yake akianza kwa kuripoti Polisi kwaajili ya usalama wake endapo mwizi atatumia vibaya simu yake, kisha akaendelea kufutilia kupitia kitengo maalum cha Polisi kinachohusika na mambo ya mitandao.

Aliendelea kufuatilia hadi mwezi Mei, 2018 ambapo alipewa taarifa na Jeshi la Polisi kuwa simu yake imeonekana inatumika na mtu mmoja Mkoani Pwani hivyo akafanya taratibu za kumpata huyo mtu na alimkuta nayo.

Ameeleza jambo muhimu la kuzingatia ni kuhakikisha unahifadhi 'IMEI' namba ya simu yako yaani 'International Mobile Equipment Identity' ambayo ndio husaidia kuangalia simu na eneo ililopo na kutambua mtu anayetumia.

Kupata kwa undani zaidi juu ya mkasa huu, endelea kufuatilia 'GUTUKA' ya East Africa Drive kila siku za Ijumaa ili uweze kujifunza mengi kuhusu umuhimu wa kufuatilia simu uliyopoteza na si kuishia kurejesha 'SIM card' na kununua simu mpya.