SACP Joseph Konyo akiwa katika msitu wa Biharamulo
Mwili wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Yohana Bahati aliyetekwa siku tatu zilizopita, umepatikana ukiwa umekatwa miguu na mikono yote na kiwiliwili chake kufukiwa shambani katika kitongoji cha mapinduzi kijiji cha Rumasa ndani ya hifadhi ya msitu wa Biharamulo wilaya ya Chato mkoani Geita.
Mtoto huyo wa mwaka mmoja alitekwa Jumapili iliyopita nyumbani kwao saa mbili na robo usiku akiwa amebebwa na mama yake mzazi, Esther Jonathan ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo kwa kupigwa panga usoni.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo, amesema mwili huo umepatikana jana saa 12:30 jioni katika shamba la mahindi lisilo rasmi kutokana na kulimwa ndani ya hifadhi ya msitu wa Biharamulo wilayani Chato.
Kamanda SACP Joseph Konyo amesema maiti ya mtoto huyo iligunduliwa na mpita njia katika shamba la mahindi lililopo kitongoji cha tatu kutoka nyumbani kwao, baada ya kuona kipande cha nguo yenye damu ambapo alipiga yowe lililowakusanya wanakijiji ndipo walifukua shimo alipokuwa kafukiwa na kukutwa akiwa hana mikono na miguu yote.
Wakati huo huo hali ya mama Ester Jonas ambaye ni mama wa mtoto huyo bado ni tete na madaktari wa hospitali ya rufaa Bugando wanaendelea na juhudi za kuhakikisha hali yake inaimarika.