Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga kamishina msaidizi Justus Kamugisha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Longinus Tibishubwamu, amesema tukio hilo limetokea juzi saa 7:30 mchana, wakati wanafunzi hao wakiwania daftari walioazima waliposababisha ugomvi mkubwa.
Tibishubwamu amemtaja mwanafunzi amefariki dunia ni Veronica Venance (12), anayesoma darasa moja na mwenzake aliyesababishia mauaji hayo.
Akizungumza na East Africa Radio jana, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Magere Jonas, amesema wakati wanafunzi hao wanagombea daftari hilo, alikuwa amepumzika chini ya mti akiwa na mwalimu mkuu msaidizi, na ghafla wakaletewa taarifa na wanafunzi wenzao wanagombana darasani.
Jonas amefafanua mara baada ya kuingia darasani wakamkuta mwanafunzi huyo akiwa amelala chini anagalagala, hivyo kuchukua jukumu la kumkimbiza kwenye kituo cha afya Bugisi jirani na shule hiyo lakini kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo alifariki dunia.
Hata hivyo, mtendaji wa kata ya Ilola, Mahona Joseph, amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza marehemu alikuwa ameng’anga’nia daftari alilokuwa ameazimwa na Sophia Mathew kwa ajili ya kuandika (notes) kitendo ambacho kilimkera mwenzake huyo na kuzua ugomvi.
Aidha, Kaimu kamanda wa polisi mkoani humo, Tibishubwamu, amesema wanamshikilia mwanafunzi huyo kwa mahojiano zaidi pamoja na kufanya upelelezi juu ya tukio hilo na uchunguzi utakapokamilika watamfikisha mahakamani ili kupewa adhabu inayostahili.