Wednesday , 20th Jan , 2016

Mwalimu wa shule ya Msingi Ikombohinga iliyopo wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, amelalamikia kuchapwa makofi na Ofisa elimu kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye semina ya kufundisha watoto stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).

Tukio hilo lilitokea baada ya mwalimu huyo kuchelewa kufika kwenye mafunzo hayo kwa takribani dakika 40 kwani alitakiwa kufika saa 2:00 lakini alifika saa 2:40 yeye pamoja na wenzake kwenye semina hiyo yenye lengo la kuwajengea watoto wa darasa la kwanza na la pili stadi za kusoma kuandika na kuhesabu.

Akielezea sakata hilo mwalimu aliYepigwa Peter Hema alisema kuwa Afisa elimu huyo amemdhalilisha kwa kumpiga kibao baada ya kuchelewa kufika kwenye semina hiyo waliyokuwa wakiifanya.

Kufuatia hali hiyo Mwenyekiti Chama Cha walimu Wilaya ya Chamwino (CWT) Clementi Mahenga alisema kuwa chama hicho kinalaani vikali tukio hilo na kuitaka serikali kuhakikisha inamchukulia hatua kali za kisheria Afisa elimu huyo kwa kukiuka kanuni na sheria za utumishi wa umma.

Alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakiitumia vibaya kauli mbiu ya Hapa kazi tu kwa kuwadhalilisha na kuwaonea watumishi wa ngazi za chini serikalini.

Alipotafutwa Afisa elimu huyo ili kuzungumzia tuhuma hizo alikanusha vikali kuwa yeye hakumpiga vibao wala hakumsukuma mwalimu huyo.

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa Chamwino Richard Masimba alipotafutwa ofisini kwake alisema taarifa hizo hawana na watazifuatilia.

Masimba alisema ofisi haina taarifa ya mwalimu kupigwa vibao na kusukumwa ukutani na iwapo itathibitika hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya Afisa Elimu huyo.