Thursday , 16th Feb , 2017

Waziri wa Sheria na Katiba Dkt. Harrison Mwakyembe ameendelea kufunguka jinsi alivyokwama kudhibiti upitishwaji wa dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati alipokuwa Waziri wa Uchukuzi hadi kuzidiwa kete na Agnes Masogange

Mwakyembe (Kushoto) mwaka 2013 akionesha jinsi Masogange alivyopita katika Uwanja wa Ndege akiwa na mzigo bila kufanyiwa ukaguzi

Waziri Mwakyembe akiwa kwenye kipindi cha East Africa Breakfast amesimulia kilichotokea wakati alipotaka kumdhibiti binti mmoja aliyedaiwa kupitisha masanduku matano ya 'materials' za kutengenezea dawa za kulevya aliyekamatwa nchini Afrika Kusini akitokea Tanzania.

Amesema baada ya kufuatilia sakata lile mbali na kuchukua hatua kwa watu waliomsaidia kupitisha mzigo uwanja wa ndege, aliamua kufanya jitihada za kumkamata binti huyo ili achukuliwe hatua, lakini muda mfupi baada ya binti huyo kurejea nchini, yeye alihamishwa wizara, hivyo kukosa nguvu ya kumshughulikia, hatua iliyofanya binti huyo kumfanyia "nyodo".

Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa ndani ya Studio za EA radio.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa binti ambaye alikamatwa nchini Afrika Kusini wakati huo kwa madai hayo, na kisha Waziri Mwakyembe kumfuatilia hadi kutimua baadhi ya watumishi wa uwanja huo Mwezi Agost mwaka 2013 alikuwa ni 'video queen' maarufu nchini, Agnes Gerald 'Masogange'.

Vilevile Mwakye amesema kijana wake mmoja anayefahamika kwa jina la Jingu ambaye yuko gerezani, anapaswa kuongezewa ulinzi kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa jemedari wa kudhibiti dawa za kulevya uwanjani hapo, lakini baadaye aliundiwa kesi na sasa huko gerezani anakutana na watu ambao wanaweza kumdhuru kutokana na kwamba yeye ndiye aliyesababisha wafungwe.

Mtazame hapa Dkt. Mwakyembe akifafanua zaidi.......