Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime
Akizungumza mama mzazi wa mtoto huyo, Carolina Mnyawami ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mingui kata ya Lumuma Wilayani Mpwapwa amesema tukio hilo limetokea leo majira ya saa 4 asubuhi ambapo mume wake aliyefahamika kwa jina la Fabian Chigoda alikuwa anapigana na kaka yake hivyo aliamua kuwaamulia ugomvi wao.
Amesema katika ugomvi huo walikuwa wanapigana na fimbo, hivyo alipowanyang’anya fimbo hiyo ili wasiendelee kupigana ndipo (Chigoda) alipoamua kuchukua mchi ili ampige nao mkewe kichwani lakini alikwepa na alipourusha ndipo ulipompata mtoto huyo kichwani.
“Nilipowanyang’anya fimbo ili wasiendelee kupigana, mume wangu aliokota mchi na kunirushia kichwani.. kwa bahati nzuri niliuona mchi huo na kukwepa ili usinipige ndipo ulipompiga kichwani mwanangu niliyekuwa nimembeba mgongoni,” amesema Carolina.
Ameongeza kuwa, “Baada ya kuona kuwa amempiga mtoto alikimbia na hajulikani alipo mpaka sasa.”
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Said Mawji amethibitisha kumpokea mtoto huyo na kwamba hivi sasa mtoto huyo anaendelea kupata tiba na uchunguzi zaidi wa afya yake.
“Ameumia sana kichwani lakini bado tunampatia tiba na uchunguzi zaidi kwenye fuvu la kichwa, kwani inaonekana kama vile limepasuka,” amesema Dk, Mawaji.
Hata hivyo amesema kuwa wanafanya mpango wa kumpa rufaa mtoto huyo ili aweze kwenda kutibiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mingui, Mwingwa Udoba amesema chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia na kwamba bado wanamtafuta baba mzazi wa mtoto huyo kwa kuwa alikimbia baada ya tukio hilo.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo simu yake ilipokelewa na mtu aliyesema kuwa Kamanda alikuwa kwenye kikao cha kazi.