Wednesday , 4th Feb , 2015

Rais Jakaya Kikwete amevitaka vyombo vya upelelezi kutokurupuka kwa kupeleka kesi mahakamani ambazo upelelezi haujakamilika matokeo yake wanashindwa kesi na kwamba huko ni kumnyima mtu haki kwa kupeleka mashitaka yasiyostahili.

Rais Kikwete ametoa rai hiyo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini ambapo amesema watanzania lazima wapate haki tena kwa wakati na kuwataka mawakili, waendesha mashitaka na vyombo vya upelelezi kufanyakazi kwa pamoja ili visiwe chanzo cha kuchelewesha mashauri pasipo sababu.

Ameongeza kuwa kama shitaka halijakamilika wasikamate watu huku akielezea hatua mbalimbali serikali ilizochukuwa katika kuboresha mfumo wa mahakama.

Naye Jaji mkuu wa Tanzania Mh Mohamed Chande Othman amebainisha baadhi ya vikwazo vinavyochangia kukwamisha ufanikishwaji wa fursa ya wananchi kupata haki kuwa ni pamoja na sheria nyingi kutokuwa kwenye lugha ya taifa kwani zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza.

Pia amelitaka bunge kuangalia namna ya kufanya ili sheria ziwe rafiki kwa watumiaji wote kwani watanzania wengi wanakosa haki kwa kutokuelewa lugha inayotumika.

Katika hotuba yake mwanasheria mkuu wa serikali Bw George Masaju amesema mahakama ndiyo kimbilio la watu wanaohitaji haki, hivyo ina wajibu wa kuwasikiliza watu wanaofungua au kufunguliwa mashauri na kutoa uamuzi kwa kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi, kutochelewesha haki, kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine.

Akisoma hotuba ya chama cha wanasheria Tanganyika TLS Rais wa chama hicho Charles Rwechungura amesema uelewa mdogo wa sheria miongoni mwa wananchi unachangia kuzuia upatikanaji wa haki ambapo ametolea mfano mkoa wa Dodoma ambako wamebaini kuwa idadi kubwa ya watu walipoteza haki zao za umiliki wa ardhi na masuala ya ndoa kwa sababu ya kutokujua njia gani watumie ili kupata haki hadi muda wa ukomo uliowekwa chini ya sheria ulipomalizika.