Friday , 8th Feb , 2019

Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa ameendeleza vita yake na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi juu ya madai ya kutumia vibaya ofisi yake na kupelekea kushusha ari ya ufanyaji kazi kwa watumishi wa umma mkoani Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi na Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa.

Mchungaji Msigwa ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akichangia kwenye mjadala juu ya utawala bora ambapo alidai kuwa baadhi ya wateule mkoani kwake wanatumia vibaya mamlaka yao ya kisheria.

Akichangia kwenye mjadala huo Msigwa amesema, "mara nyingi tumeambiwa kwamba hatusifu ila nimeamua kutoa sifa zifuatazo, kwanza nampongeza Mkuchika kutoa semina ya utawala bora Mkoa wa Iringa, na ninashangaa kuona viongozi wengine wakiendelea kutofuata utaratibu wa Mkuchika."

"Hawa Wakuu wa Mikoa wengine wanapagawa sana wanafika hawamjali mtu yeyote ikiwezekana Waziri Mkuu na TAMISEMI muendelee kuwalea hawa vijana kwa sababu haya mambo ya kuwaweka watu ndani yanashusha ari ya kufanya kazi", ameongeza Msigwa.

Wakati Mbunge Msigwa akisema hayo, Mbunge wa Chemba Juma Nkamia alibainisha kuwepo kwa tatizo kama hilo wilayani Chemba ambapo zaidi ya watumishi 30 alidai waliomba kuhamishwa kwa sababu viongozi wao kuwa na matumizi mabaya ya madaraka.