Tuesday , 28th Jul , 2015

Vyama vya siasa 21 vinavyotarajiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani baadaye mwaka huu vimesaini Maadili ya Uchaguzi yatakayotumika wakati wa kampeni, kupiga Kura na wakati wa kutangaza matokeo.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva

Maadili hayo yanayohusisha Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Vyama vya Siasa yalisainiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dr. Florence Turuka, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva na Wawakilishi wa Vyama vya Siasa 21 nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume Jaji Damian Lubuva amesema Chama cha Wananchi (CUF) hakikusaini Maadili hayo kutokana na kuwa na kazi nyingine lakini akasisitiza kuwa Chama hicho kitasaini
Maadili hayo wakati wowote.

Akifafanua kuhusu Maadili hayo, Jaji Lubuva alisema Maadili yanapaswa kuanza kutumika rasmi Agosti 22 mwaka huu wakati kampeni za uchaguzi zitakapoanza, katika kipindi cha kupiga Kura na wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.

Alisema maadili hayo pia yatahusu wajibu wa vyama vya siasa na wagombea na mambo yasiyotakiwa kufanywa na vyama vya siasa na wagombea.

Maadili pia yatahusu masuala yanayotakiwa kufanywa na yasiyotakiwa kufanywa wakati wa kupiga Kura.

Jaji Lubuva aliongeza kuwa Maadili yaliyosainiwa pia yatahusu maadili kwa tume ya uchaguzi yaani mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanywa na tume hiyo.

Aidha, Maadili hayo yatahusu mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanywa na Watendaji wa serikali katika kipindi chote cha uchaguzi.